Friday, May 22, 2009

unaweza nyoni

ERASTO NYONI EDWARD:

Beki Stars anayetamani safari yake ya nje ianzie Rwanda

na said makala

NI miongoni mwa wachezaji chipukizi wa mwanzo mwanzo kuitwa tokea mikoba ya kuinoa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars iwe mikononi mwa Mbrazil, Marcio Maximo.
Alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka juzi akiwa na Vital’o ya Burundi, hakuwa mchezaji anayefahamika sana nchini licha ya ukweli kuwa aliwahi kuichezea AFC ya Arusha iliyoshiriki ligi kuu ya Vodacom, msimu wa 2005.
Lakini bao lake lililoipatia ushindi Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso wakati wa kusaka nafasi ya kufuzu kwa kombe la Mataifa ya Afrika, 2008 alilofunga ugenini jijini Ouagadougou, ndilo hasa lilimjengea jina kubwa nchini Tanzania.
Kwa sasa, Nyoni ambaye ni mzaliwa wa Songea mkoani Ruvuma ni mchezaji wa kikosi cha Azam FC kilichokuwa chini ya Mbrazil, Neider Dos Santos na msaidizi wake, mzawa Sylvester Mash, akiwa na mkataba wa mwaka mmoja unaomalizika Agosti mwaka huu.
Mara nyingi amekuwa akicheza kama mlinzi wa kati au pembeni kushoto, lakini katika mazoezi ya Taifa Stars yanayoendelea hivi sasa ikijiandaa kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya New Zealand, Nyoni anachezeshwa kama beki wa kulia, nafasi ambayo inamilikiwa na Shadrack Nsajigwa katika kikosi hicho.
Akiwa amezaliwa Julai 7, 1983 (Sabasaba), alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Mahenge iliyopo mjini Songea kuanzia mwaka 1993 hadi alipomaliza 2000. Kutokana na matatizo mbalimbali, hakufanikiwa kuendelea na elimu ya Sekondari.
Kama ilivyo kwa wanasoka wengi, alianza kupenda soka akiwa na umri mdogo lakini hasa aliweza kuibuka pale alipochaguliwa katika timu ya shule katika michezo ya UMISHUMTA, akiwa darasa la nne.
Kufuatia kuonyesha kipaji cha juu katika michezo hiyo, Nyoni aliweza kuwavutia mashabiki wengi na kaka yake, anayemtaja kwa jina la George, aliahidi kumpeleka katika timu aliyokuwa akiichezea, iliyoitwa Five Star.
“Kweli nilioneka ni mtoto mdogo lakini niliweza kucheza vizuri. Na kweli alinipeleka lakini kutokana na umri wangu kuwa bado mdogo, nilikuwa sichezi mechi zaidi ya kufanya mazoezi na wakubwa,” anasema Nyoni.
Alipomaliza darasa la saba, ndipo akajiunga rasmi na timu hiyo na kukaa nayo kwa muda wa mwaka mmoja, akicheza ligi ndogo ndogo zilizokuwa zikiandaliwa na watu mbalimbali kwa zawadi za fedha.
Ni ligi hizo ndizo zilizomweka katika kiwango kizuri kwani siku moja, kaka yake aliyekuwa akiishi Arusha wakati huo, alimtumia ujumbe kumtaka kwenda mkoani humo akajaribu bahati yake katika mashindano yaliyoandaliwa na shule ya vipaji ya Rolling stone Football Academy.
Mashindano hayo yalishirikisha wachezaji chipukizi kutoka nchi za Burundi, Kenya, Zanzibar na vyuo mbalimbali.
Alifurahia wito huo na kuamini kuwa wakati wa kutimiza ndoto zake za kusakata kandanda kwa kiwango kikubwa ulikuwa umewadia.
Na ikawa kweli kwani alionyesha uwezo mkubwa wa kucheza soka na kuisaidia timu yake ya Rolling stone kuibuka mabingwa, hali iliyopelekea kupata nafasi ya kusajiliwa na AFC.
Alikuwa ni kocha wa AFC wakati huo ikishiriki ligi kuu, Hali Mtumwa ndiye aliyemdokeza nia yake ya kumtaka aichezee timu yake, jambo ambalo alilikubali mara moja.
Mwaka mmoja baadaye, viongozi wa soka wa Burundi, ambao waliwahi kumuona kwenye mashindano yale ya vipaji, walimfuata na kumweleza lengo lao la kumtaka kuelekea nchini humo kwa ajili ya kucheza soka.
Kocha wake Mtumwa, hakuwa na kinyongo kwani alimruhusu na hivyo kumfanya Nyoni kuvuka mpaka hadi Burundi alikojiunga na Vital’o.
Katika safari hiyo, aliandamana na mtoto wa kocha huyo, Abdalah Hali ambao wote walisajiliwa na miamba hiyo ya Burundi.
“Majaribio yalienda vizuri, nilikubalika na tukatiliana mkataba wa miaka miwili na nusu ambapo katika miaka hiyo ya 2006 na 2007 niliweza kuisaidia timu hiyo kuwa mabingwa mara mbili mfululizo,”
“Msimu wa 2008 ulipoanza nilicheza nusu tu, nikaondoka na kuja kujiunga na Azam ambayo nimesaini nayo mkataba wa mwaka mmoja unaomalizika Agosti mwaka huu,” anasema Nyoni.
Moja ya sababu kubwa iliyomrejesha nyumbani, ni kutaka kwake kuonekana ili aendelee kuitwa kikosi cha Stars, ingawa pia upinzani wa ligi kuu ya Vodacom umechangia.
“Wazo la kucheza nje lipo lakini sio kwenda katika nchi kubwa kisoka, nataka nianzie karibu ili kujiweka fiti kwanza na nchi ya kwanza ni Rwanda maana wananitaka sana kwani nilishawahi kufanya mazungumzo nao na waliridhia kauli yangu ya malipo hivyo natarajia mkataba wangu ukimalizika na Azam nitaenda kujaribu bahati yangu,”anasema.
Akiwa kikosi cha Vital’o, alicheza pamoja na wachezaji kadhaa Watanzania, ambao ni pamoja na Abdalah Hali, Abdalah King’alu, Stainless Minzi na Hafivi Mussa, ambao hata hivyo, kwa sasa wote wamerejea nyumbani.
Kuhusu mchezaji wa nyumbani anayemvutia, mchezaji huyo anasema kwa kujiamini.
“Hakuna kama Haruna Moshi ‘Boban’. Anaweza mpira, ana kipaji chake cha kipekee na ananivutia sana, kama ananisikia kaka yangu huyo ajaribu kutulia, anaweza sana, pia ajaribu soka Ulaya anaweza kufuzu bila vipingamizi kwani uwezo wake ni wa kiwango kikubwa,”anasema.
Anasema wakati kiungo huyo mahiri alipokuwa Stars kabla ya kutemwa alikuwa mfano mkubwa kwake, kwani anapokuwa uwanjani huonyesha kilichompeleka na anakiri kumuiga kiungo huyo nyota wa Simba kiuchezaji.
Kwa nje, Nyoni anavutiwa na kiungo wa Barcelona ya Hispania, Andreas Iniesta pamoja na Xavi Hernandez na kusema ni wachezaji wenye kiwango cha juu kuliko hata Ronaldo.
Anasifu ushirikiano kati ya Iniesta na Lionel Messi wawapo uwanjani kwani mmojawapo asipokuwepo, mwenzake huonekana kuwa na huzuni.
Si soka pekee linalomkuna beki huyu bali anavutiwa pia na muziki wa kizazi kipya, hasa mzee wa Commercial, Ambwene Yessaya ‘AY’.
Huyu ndiye Erasto Nyoni Edward, beki ambaye Maximo anamwandaa kwa ajili ya kuiua New Zealand mwezi ujao.

No comments: